Monday 30 June 2014

Usisubiri mpaka afikirie kutafuta wa kumtuliza!


NILIWAHI kuandika kabla, leo narudia tena, jinsi unavyoishi leo ni matokeo ya ulivyokuwa ukiishi zamani. Kama unaishi maisha magumu na tabu zinakuandama kila kona, vuta picha uangalie miaka mitano nyuma ulivyokuwa ukiishi.
Rafiki zangu, pointi kubwa hapa ni kwamba, unatakiwa kuangalia kila hatua

ya maisha yako ya sasa kwa maana ni mtaji wa jinsi utakavyoishi siku zijazo. Ukiwa mtu wa kuwaombea wenzako mabaya, kuwasengenya, kuwasimanga, kuwadharau, kukatisha tamaa n.k, majibu yake utayapata baadaye!
Ukimchukia binadamu mwenzako leo kwa sababu ana vitu ambavyo huvipendi au sababu zako binafsi
ni wazi tayari mtakuwa mnatengeneza uadui. Kama ndivyo, kesho anaweza kukusaidia? Jaribu kuvuta picha, unakorofishana na watu wawili kila mwezi, maana yake kwa mwaka utakuwa na watu 24 ambao hamzungumzi! Hebu zidisha mara miaka mitano. Utaishije?
Tukiachana na hilo, hebu twende katika mfano mdogo sana wa kawaida; Utakuta mtu leo hii anatumia fedha zake hovyo kwa kulewa na anasa nyingine zisizo na maana, haweki akiba na mipango ya matumizi ya fedha, miaka kumi ijayo atakuwa wapi? Bila shaka atakuwa akipata shida analalamika na kuanza kukumbuka maisha yake yaliyopita. Utamsikia: “Niliwahi kufanya kazi wizarani, nilikuwa na nafasi nzuri sana....yule nanii tulisoma naye...”
Itakusaidia nini? Kujisifu kuwa mtu fulani maarufu ulisoma naye au ulifanya naye kazi katika kitengo fulani nyeti itasaidia nini? Angalia umesimamia wapi? Rafiki zangu, kama ukisoma maneno haya kwa maana ya kupima na kuyafanyia kazi, huwezi kujuta siku zijazo za maisha yako. Msingi mzuri wa kesho, huanza kujengwa leo. Hii ipo hata katika mapenzi, unakorofishana na mpenzi wako leo, mnagombana na kuachana. Kesho akienda kuoa au kuolewa na mwingine, unaanza kujilaumu. Haitakusaidia kitu ndugu yangu. Jipange na ufanye kila kitu katika maisha yako huku ukiangalia mustakabali wako wa kesho.
Unapokuwa kwenye ndoa, lazima ujue kusoma alama za nyakati. Kuna wakati mambo yanaweza kubadilika ndani ya nyumba, lakini kuna taratibu fulani ukianza kuona kama zinataka kujirudia ujue kabisa kuna kitu kinatakiwa. Nazungumzia suala la tendo la ndoa. Wapo watu walioumbwa tofauti.
Wengine wanaweza kusema wazi kabisa: “Leo mama nanii nataka,” mwingine akasema: “Dear leo nina hamu sana na wewe,” lakini wapo ambao hawawezi kusema chochote! Vitendo vinaongea...
Hawa ndiyo ninaowazungumzia leo. Rafiki zangu, ukiwa na mwenzi wa aina hii na usipokuwa makini kujua kuwa mwenzako anakuhitaji ni rahisi kumuacha na kiu yake, lakini wakati huo ukawa unamwachia mlango wa kutafuta mwingine ambaye anaamini ataweza kutuliza maruhani yake kwa wakati.
Wenye tatizo hili hasa ni wanawake; Wanaume wengi si waoga kusema wanawahitaji wenzi wao faragha. Tena wao ndiyo huwa waanzilishi wa kila kitu. Anaweza kutoka kazini akiwa hana wazo kabisa na jambo hilo, lakini akifika nyumbani ghafla anajisikia kukutana na mwenzake.
Hafikirii mara mbili, ataanza visa na michezo midogomidogo, mwishowe kazi inakamilishwa. Ndivyo walivyo. Kazi ipo kwa wanawake ambao sasa wapo katika makundi matatu; Machakaramu wanaoweza kusema moja kwa moja WANATAKA, wanaozungumza kwa vitendo na wale wakimya wanaosikilizia amri kutoka mwanaume.
Makundi yote haya yanahitaji umakini mkubwa. Athari kubwa ni kwamba ni rahisi kusalitiwa kama hutakuwa makini katika kuchunguza alama za nyakati na uhitaji wa mwanamke wako. Rafiki zangu, ndoa ni kitu ghali kuliko kingine chochote duniani.
Ni agano ambalo linatakiwa kuheshimiwa, kulindwa na kupewa kipaumbele. Hata kama una kazi nzuri, ikiwa nyumbani kwako kuna tatizo, cheo chako si chochote. Kama mke wako analalamika humfurahishi kiasi kwamba anaanza kufikiria kutafuta mtu mwingine nje ni tatizo.
Nimeanza na dodoso rafiki
zangu, wiki ijayo tutaingia kwenye mada yenyewe ambapo tutaangalia kwa kina makundi hayo na tabia zake.
Kidogo ina mambo yake lakini nitajitahidi kuzungumza kwa lugha ya kirafiki zaidi ili ujumbe ufike vyema bila kuharibu hali ya hewa.