Friday 27 June 2014

MZUNGUKO WA HEDHI (MENSTRUAL CYCLE)

 
MZUNGUKO UNAOPEVUSHA MAYAI
MZUNGUKO huu kitaalam unaitwa ‘Ovulatory cycle’ pia unaweza kuwa mfupi mrefu au wa kawaida kama tulivyoona katika sehemu iliyopita.

Mwanamke mwenye mzunguko huu hupata ute wa uzazi katikati ya mzunguko, yaani vile vipindi anavyoweza kushika mimba kwa mujibu wa kalenda.
Ute wa uzazi umegawanyika katika makundi matatu. Ute mwepesi, ute mwepesi na  unaovutika na ute mzito.
Ute huu wa aina zote kwa ujumla hutoka kati ya siku nne hadi tano.
Katika kipindi cha upevushaji mayai, pamoja na kupata dalili za ute wa uzazi joto la mwili pia huongezeka kidogo, matiti hujaa na pia hupatwa na maumivu kidogo chini ya tumbo. Wapo wengine hutokwa na damu kidogo.
Ovulation au upevushaji pia unaweza kugundulika kwa vipimo maalum endapo mwanamke haoni ute wa uzazi labda unatoka kwa kiasi kidogo sana.
Matatizo ya kisaikolojia kuwa na hamu sana ya kupata mimba au kukata tamaa ya kupata mimba pia huathiri upevushaji.
Yapo matatizo mengine yanayoambatana na kasoro au hitilafu mbalimbali katika mfumo wa uzazi.
Kutopevusha mayai kuna sababu nyingi ambazo tutakuja kuziona katika matoleo yajayo na jinsi ya kufahamu tarehe maalum za kushika mimba na siku za kupata mtoto wa kiume au wa kike kimahesabu.

Mabadiliko katika mfumo wa hedhi pia huachangiwa na hali ya hewa, ‘stress’, matumizi ya madawa, maambukizi na sababu nyingine nyingi ambazo tutakuja kuziona.
Matatizo katika mfumo wa hedhi
Matatizo haya ni kama vile
kutopata hedhi hali iitwayo kitaalam ‘Amenorrhea’, maumivu wakati wa hedhi ‘Dysmenorrhea’ na kupata damu bila ya mpangilio.
Matatizo haya yanaweza kusababishwa na hitilafu katika mfumo wa homoni au maambukizi ya kizazi.
Dalili za maambukizi ya kizazi ni kuwa na maumivu ya tumbo chini ya kitovu kwa muda mrefu, kutokwa na uchafu ukeni unaoambatana na muwasho na harufu, maumivu wakati wa tendo la ndoa na kupoteza hamu ya tendo la ndoa.
Kutokwa na damu yenye mabongebonge na nyingi pia siyo dalili nzuri.

Uchunguzi

Hufanyika katika hospitali za mikoa kwa madaktari wa magonjwa ya kinamama, vipimo mbalimbali hufanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa.
Matibabu na ushauri
Hutegemea na chanzo cha tatizo kwa hiyo ni vema mhusika akajieleza vizuri
kwa daktari wake. Ni vema endapo unatafuta ujauzito basi uwe na sehemu moja maalum ambapo daktari wako atakuwa anakufuatilia hatua kwa hatua ili kujua tatizo na jinsi ya kulishughulikia.