Wednesday 13 May 2015

USIJIDANGANYE MWANAUME HAKOMOLEWI!

Haya weee, mimi nipo poa unashangaa nini kujibu majibu ya kisasa, mbona hujishangai wewe mama mtu mzima kushindana kwenda utupu na binti yako, sasa likiharibika nani amkanye mwenzake. Hebu nipishe huko ushaanza kukunja domo kama dege lililokosewa kumwagwa. Umenuna umecheka habari ndiyo hiyo. 

Leo, shoga yangu nazungumza na wewe mwanamke usiye na haya usiyejua wakati gani wa kumkomoa mumeo, jamani wanawake wengine sijui tumerogwa na mchawi aliyeturoga kaugua wendawazimu sijui nani wa kutuponya.Kuna kitu kimoja jana kilinikera na kunifanya niwarudishe kwenye unyago, nikiwa nakwenda zangu mjini nilipanda kwenye daladala na kukaa siti ya nyuma, mbele yangu kulikuwa na wanawake wawili waliokuwa wakiongea mambo ya ndani bila aibu. 

Kutokana na maongezi yao ndiyo maana nikajiuliza kama waliochezwa wamesahau mafunzo ya unyagoni itakuwa wewe unayewekwa masaa mawili mbele ya watu eti Kitchen party! Hivi kwanza wewe mwanamke, eeh jamani aibu umeiweka wapi kufikia hatua ya kuyasema maneno ya ndani mwako ndani ya daladala bila hata kugongwa na mshipa wa aibu. 

Nilimsikia akisema eti alikorofishana na mumewe na kumsubiri kitandani ndipo alipomkomoa kwa kumkaripia alipomgusa na kumwambia amkome.Weweee mwanamke ndivyo mlivyofundishwa unyagoni kumfanyia mumeo kitandani pale mnapokosana. Unajua madhara ya kumnyima mumeo kata ya maji ukweni akiwa na kiu kikali? 

Kibaya zaidi upumbavu ulioufanya unamweleza rafiki yako, pengine hata hajui ndoa ni nini, majibu yake mepesi. “Shoga tena mkomeshe, wanaume wamezidi.”Hizi ndizo moja ya sababu za kumfanya mumeo atembee na house girl, pengine kafikisha umri wa kutumwa sokoni akarudi. 

Wewe umekataa pengine wiki ukijua unamkomoa, mwanaume hakomolewi shoga, tupo day worker kibao tunatafuta kazi hata ya masaa, telekeza gari day worker alikamate kama tajiri atakukumbuka.Nataka tuzungumze kitu kimoja kwako wewe mwanamke, ni kosa kufungua mahakama kitandani, mwenzio anataka wewe ndiyo unaanza “unajua,” ajue nini mpe haki yake mashtaka baadaye. 

Shoga, unamnyima mumeo haja zake akamalize wapi, akipata nyumba ndogo inayomjali uanze kupiga kelele. Hebu wanawake tuache akili za punda wa dobi, mumeo akikukosea pataneni lakini siyo kumpa adhabu ya kumnyima chakula cha usiku.Kwa leo ni hayo tu.