Tuesday 29 August 2017

Zifahamu dalili za ugonjwa wa saratani

Saratani ni ugonjwa unaotokana na kushindwa kudhibiti ukuaji wa chembe mwili. Saratani hudhuru mwili kwa chembe zilizoathirika zinapogawanyika bila utaratibu unaofaa na kuweka mikusanyiko ya uvimbe ya chembe hai.

Uvimbe huo mara nyingi huwa hauna maumivu na hukua kabla ya kuingilia kwenye mifumo ya unyeyushwaji wa chakula, mfumo wa fahamu kwa ufanisi na kutoa homoni zenye kudhuru ufanyaji kazi katika mwili wa binadamu.

Ugonjwa huu ni matokeo ya kukua na kutokufa kwa chembe hai, Kwani kawaida chembe mwilini hufuata taratibu maalum za kukua, kugawanyika na kufa ambapo utaratibu wa kufa kwa chembe kitaalamu unaitwa “apoptosis”.

Pindi mchakato huo unapofanyika, ndipo saratani hujitengeneza na ni tofauti na mfumo wa kawaida wa chembechembe, chembembechenbe za saratani hazifuati utaratibu wa kufa na huendelea kukua na kujigawanya hali ambayo hufanya kuwepo kwa chembe nyingi zisizokomaa zinazokuwa nje ya utaratibu.

Zipo dalili ambazo ukiziona ni vyema kwenda kwa mtaalamu wa maswala ya afya kwa ushauri zaidi, dalili moja wapo ni upungufu wa uzito usioelezeka, watu wengi wenye dalili za ugonjwa wa saratani hupoteza uzito kwa kipindi fulani
Unapopoteza uzito kwa kutojua sababu, hali hii huitwa kupungua uzito kusikoelezeka kupungua uzito usioelezeka wa pauni 10 au zaidi kunaweza kuwa sababu za awali za ugonjwa wa saratani.

Dalili nyinginea ya ugonjwa wa saratani ni unyong’onyeaji, hali hii inaweza kuwa ni moja ya kukua kwa saratani kwani inaweza kutokea mapema kwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

Maumivu yasiyopona kwa muda mrefu ni dalili nyingine ya ugonjwa wa saratani, mfano mvutaji wa sigara anapopata maumivu ya mdomo kwa mda mrefu huashiria ni dalili ya ugonjwa huo na watu wanaotumia sigara wapo katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa saratani.

Pia karibu wagonjwa wote wenye saratani huwa na homa kwenye vipindi tofauti, hasa kama saratani yenyewe au tiba yake inaathiri mfumo wa kinga ya mwili, hali hii inatokana na mwili kushindwa kuwa na uwezo wa kukabiliana na maambukizi.

Ugonjwa wa saratani ni ugonjwa ambao umuathiri sana binadamu, ni vizuri uonapo dalili hizi kuweza kwenda kwenye vituo vya afya kwa ushauri zaidi na kujua kinga ya ugonjwa huu ni muhimu sana kwani itasaidia kupunguza maambukizo ya ugonjwa huu nchini.