Thursday 31 August 2017

Kimenuka: Chadema yatangaza mgogoro na serikali

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza mgogoro na mkuu wa wilaya ya Momba, Juma Irando kwa kuagiza jeshi la polisi wilayani humo kumuweka ndani kwa saa 48 mbunge wa Jimbo la Tunduma, Frank Mwakajoka kwa madai ya uchochezi.

Katika kikao alichofanya na wanahabari, Mwenyekiti wa CHADEMA, Halmashauri ya mji wa Tunduma, Ali Mwafongo ameleezea kusikitishwa na amri hiyo ya mkuu wa wilaya na kusema kuwa kamwe hawatarudi nyuma huku akiahidi kutompa ushirikiano mkuu wa wilaya huyo.

"Uchungu tunaopata sasa hivi tunajua ipo siku itakuwa furaha kwetu kwani ushindi unakaribia. Kinachofanywa sasa hivi wakumbuke ipo siku watawala watakuwa wapinzani na haya yanayofanywa hayataweza kuturudisha sisi nyuma. Viongozi wetu wamekuwa wakipelekeshwa sana lakini katu hatutokata tamaa kwa sababu ni kazi yetu kusema ukweli na kuwatumikia wananchi wetu" alisema
Mbali na hayo mkuu huyo wa wilaya pia ametuhumiwa kutoa amri ya kushusha bendera za chama hicho hali ambayo imeonesha kuwakera baadhi ya viongozi wakiwemo madiwani.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Irando amekiri kutoa amri ya kukamatwa kwa mbunge huyo kwa madai kuwa ametoa kauli ya kudharau mamlaka ya uteuzi.

Mbunge Mwakajoka amekamatwa jana Jumanne na kuwekwa ndani ikiwa ni siku moja tu baada ya Mbunge mwingine wa Jimbo la Vwawa, Paschal Haonga kukamatwa na jeshi la polisi.