Wednesday 30 August 2017

Viongozi wa Afrika wakosolewa kwa matibabu ya nje

 
Waziri mmoja nchini Afrika Kusini, amewakosoa vikali viongozi wa Bara Afrika ambao wanakwenda ng`ambo kutafuta matibabu.

Aaron Motsoaledi amewalaani viongozi hao na kuwaita "Watalii wa kiafya". Amesema hayo akiwa Zimbabwe.

Rais Robert Mugabe, ambaye mara kwa mara anapokea matibabu nchini Singapore, alikuwa ameondoka kutoka katika, mkutano huo unaohudhuriwa na mawaziri wa afya, ndipo Dkt Motsoaledi, alipotoa matamshi hayo.

Msemaji wa Bwana Mugabe, alikuwa amesema kuwa Daktari wa kibinafsi wa Rais Mugabe ''sio tu raia wa Zimbabwe," ni mtu mweusi.....Na ni mweusi, mweusi mweusi sana".

George Charamba, alsema hayo alipokuwa akihojiwa na gazeti la serikali ya Zimbabwe - The Herald, mwezi Mei mwaka huu, akisisitiza kuwa Rais Mugabe kamwe haipi kisogo sekta ya matibabu ya nchini hiyo.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na mwenzake wa Angola José Eduardo dos Santos pia wamekosolewa vikali kwa kutafuta matibabu nje ya nchi mwaka huu.

Katika kongamano hilo wiki hii Dr Motsoaledi alisema:
"Sisi ndilo bara pekee duniani, ambalo viongozi wake wanatafuta matibabu matibabu katika mataifa ya kigeni yaliyoko nje ya bara hili, nje ya eneo letu. Inafaa tuaibikia hilo."

"Hii inaitwa utalii wa kiafya. Tunafaa kuboresha na kupigia debe kilicho chetu," aliongeza.
Dkt Motsoaledi pia ameiomba mataifa ya Afrika kuongeza ufadhili wa kifedha kwa sekta ya matibabu.

Amepongezwa mno na raia nchini Afrika Kusini kwa kutumia hospitali za umma badala ya hospitali za kibinafsi.

Orodha ya majina ya Marais wa Afrika waliokwenga ngambo kwa matibabu ni:


Robert Mugabe, Zimbabwe
Muhammadu Buhari, Nigeria
José Eduardo dos Santos, Angola
Patrice Talon, Benin
Abdelaziz Bouteflika, Algeria
Wakati Dkt Motsoale, alipotoa matamshi hayo wakati wa vikao vya kongamano hilo, kulikuwa na ukimya kutoka kwa wanachama wa mataifa yaliyowakilishwa.

Dkt Motsoaledi alikiri kuwa msimamo wake una utata, lakini aliamua kusema kindakindaki.