Tuesday 29 August 2017

Mchezaji huyu hajawahi kufunga goli ndani ya mwezi wa nane

Kibongo bongo wanaita “gundu” wakimaanisha laana, baasi Harry Kane ana gundu kubwa na mwezi wa August kwani pamoja na kuwa kinara wa ufungaji katika ligi kuu ya Epl mara mbili mfululizo na klabu yake ya Tottenham lakini Kane hajawahi kufunga August.

Katika mwezi huu ambao mara nyingi ndio pazia la ligi kuu nchini Uingereza hufunguliwa, Muingereza huyo ameshacheza dakika 893 katika michezo 13 ya ligi lakini hajawahi kutikisa nyavu hata mara moja katika mwezi huo.

Kane amepiga mashuti 44 langoni kwa wapinzani wanaokutana na Tottenham lakini mashuti yote hayo yamekuwa yakiishia mikononi mwa magolikipa huku mengine yakitoka nje ya lango.

Mbaya zaidi kwa mshambuliaji huyo hatari ni kwamba katika mashuti 44 aliyopiga langoni mwa wapinzani ni mashuti 10 tu ambayo yalikuwa on target na gundu lake na mwezi huu lilithibitika katika mchezo wao wa pili msimu huu dhidi ya Chelsea ambapo alishambulia sana na mwisho akashuhudia wakifa 2 kwa 1.

Msimu huu katika michezo miwili tu dhidi ya Chelsea na ule wa Burnley amepiga jumla ya mashuti 18, ambapo 10 aliyapiga langoni mwa Chelsea huku 8 akiyapiga kuelekea langoni mwa Burnley lakini yote hayo hamna kitu Kane hajafunga hata.

Lakini Kane amekuwa akiwaumiza sana wapinzani wao baada ya mwezi wa 8 kuisha ambapo amekuwa kila mwezi kuanzi mwezi wa 8 unapoisha amekuwa akifunga mabao kuanzia matatu kwenda juu.

Na balaa kubwa sana kwa wapinzani huwa unapofika mwezi wa 10 ambapo tathimini zinaonesha kuanzia mwezi huo ndio ambao Kane huwa anafunga mabao mengi sana na October hadi May ndio miezi Kane inayompa kiatu cha dhahabu.