Thursday 31 August 2017

Mghana apewa viatu vya Okwi

KOCHA MKUU WA SIMBA MCAMEROON, JOSEPH OMOG.
KOCHA Mkuu wa Simba Mcameroon, Joseph Omog, amesema anatarajia kumtumia mshambuliaji wake, Mghana Nicholas Gyan "kuvaa viatu" vya Emmanuel Okwi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC itakayopigwa Septemba 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Okwi na beki wa kati wa mabingwa hao wa Kombe la Shirikisho wameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda (Cranes) kwa ajili ya kuwakabili Misri ‘Mafarao’ katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018 itakayopigwa Kampala leo na kurudiana ugenini Septemba 5, mwaka huu.

Gyan (19), anatarajiwa kurejea nchini keshokutwa kuanza kuitumikia rasmi klabu yake mpya baada ya kumaliza mkataba wake na Dwafts inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana.

Akizungumza na gazeti hili jana, Omog alisema anaamini mshambuliaji huyo ana uwezo wa kuongoza safu ya ushambuliaji na kuisaidia timu yake kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo wa pili msimu huu.

Omog alisema kuwa mbali na kiwango ambacho anacho mshambuliaji huyo, pia kutofahamika vyema na mabeki wa hapa nchini ni jambo la ziada ambalo wanalitegemea kwenye mchezo huo.

"Nafikiria Gyan anaweza kuchukua nafasi ya Okwi, ni mwepesi na ana uwezo wa kuwatoka mabeki wa timu pinzani, anaweza kucheza nafasi zaidi ya mbili uwanjani, naamini kama atakuwa amefika, ataisaidia timu kufanya vizuri," alisema Omog.

Aliongeza kuwa hata hivyo anawaamini wachezaji wake wengine waliobakia kwenye kikosi hicho kwa sababu ya ushindani wa kuwania namba wanavyochuana kwenye mazoezi ya timu hiyo.

"Ni nafasi nyingine ya mastraika waliobakia kuonyesha wanaweza, kila mmoja amesajiliwa, ili kuipa timu matokeo mazuri, naamini watadhihirisha wanaweza kuwa kwenye klabu hii," aliongeza kocha huyo.

Mbali na Waganda hao wawili, pia nyota wengine sita wa Simba wako katika timu ya Taifa (Taifa Stars) ambayo inajiandaa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Botswana keshokutwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.