Wednesday 30 August 2017

Shule 29 zafungiwa Manispaa ya Ubungo

Shule 29 za msingi na awali katika Manispaa ya Ubungo zimefungiwa kwa kukosa usajili baada ya ukaguzi unaoendelea wa kukagua shule zote katika Manispaa hiyo .

Afisa Habari wa Manispaa ya Ubungo Bornwell Kapinga amesema zoezi hilo lilianza juzi na kuwa baada ya kubaini shule hizo hazina usajili walizifungia hadi hapo zitakapofuata taratibu za kusajili.

"Ukaguzi huu ulifanywa kwa kushirikiana na Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Ubungo, Chausiku Masegenya ambapo waliwaagiza wamiliki shule hizo kufuata taratibu za usajili na endapo hamtafanya hivyo wahamisheni wanafunzi na muwapeleka katika shule nyingine. Natoa wito kwa wamiliki wote wa shule mfuate taratibu pindi mnapotaka kuwekeza kwenye elimu kwani ubora wa elimu unaanzia katika usajili", alisema Bornwell.

Pamoja na hayo, Bornwell amesema lengo la kufanya ukaguzi huo ni kuboresha elimu katika manispaa hiyo lakini pia kudhibiti utitiri wa shule lukuki ambazo zimekuwa zikifunguliwa kiholela katika manispaa hiyo ambazo pia hazina ubora unaotakiwa.

Kapinga pia amewataadharisha wazazi kuandikisha watoto wao katika shule zisizosajiliwa na kuwa manispaa itatoa matangazo kwenye tovuti na kwenye mitandao ili kuonyesha wananchi shule za manispaa zilizosajiliwa .

Manispaa ya Ubungo ina jumla ya shule za msingi zilizosajiliwa zipatazo 127 ambapo shule 63 ni shule binafsi na shule 64 ni za serikali.