Saturday 23 September 2017

Mwanafunzi mbaroni, ukodishaji silaha

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Robson Maji (21) kwa kupatikana na bastola aina ya Beretta akijiandaa kuikodisha kwa Sh400,000 kwa watu wanaosadikika kuwa ni majambazi.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi, Lazaro Mambosasa leo Ijumaa kuwa, Maji ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea, ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha usimamizi wa Fedha alikamatwa Jumatano saa 2:30 usiku eneo la Mwenge akitaka kukodisha silaha.

Kamanda Mambosasa amesema bastola hiyo ilikuwa na risasi sita ndani ya magazini. Amesema awali walipata taarifa kuwa kuna watu wanakodisha silaha kwa majambazi ili wafanye kazi za uhalifu na kulipwa fedha, hivyo uliandaliwa mtego eneo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mwenge na kumkamata mtuhumiwa akitaka kukodisha kwa Sh400,000 huku akiwa tayari kuiuza kwa Sh2.5 milioni.

“Inavyoonekana silaha aliiba kwa baba yake Issack Maji (51), ambayo naye si ya kwake. Tunataka kujua aliipata wapi hivyo tumewakamata wote,” Mambosasa.

Kamanda Mambosasa amesema baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikiri kushirikiana na rafiki yake Patrick Kilosa katika kukodisha kwa wahalifu silaha hiyo ili kujipatia kipato.

Aidha ameeleza kwamba ufuatiliaji ulifanyika na kumkamata Kilosa (22) ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Columbus State Community cha Marekani, mkazi wa Tabata Segerea.

“Upelelezi unaendelea ili kujua mmiliki halali wa silaha hiyo na mahojiano zaidi yanafanyika ili kubaini silaha hiyo imekodishwa mara ngapi na imetumika na watu gani,” amesema.