Monday 25 September 2017

Anna Mghwira atoa agizo Arusha

Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amemuagiza mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, kufanya mazungumzo na kampuni ya Hodhi ya mali za Reli (Rahco) kuepusha bomoa bomoa eneo la Pasua.


Kampuni ya Rahco imewawekea alama X wananchi zaidi ya 90 wa eneo hilo kikiwamo kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL), kikiwataka waondoke eneo hilo kwa kuwa ramani ya miaka ya 1960 inaonyesha ni eneo lao.


Hata hivyo, wananchi hao wanadai wao sio wavamizi bali waligawiwa viwanja katika eneo hilo na Manispaa ya Moshi kati ya 2005 na 2010 baada ya Manispaa kubadili matumizi ya eneo hilo na kuwa makazi.


Mchakato wa kubadili matumizi ya eneo hilo ambalo katika miaka hiyo ya 1960 lilikusudiwa kujengwa kipande cha reli kwenda eneo la viwanda, yalipata baraka za wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.


Hata hivyo, eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya viwanda ambako reli hiyo ingeenda kama ingejengwa, limevamiwa na wananchi na limejengwa makazi na kufanya reli hata kama itajengwa, isiwe na pa kwenda.


Mghwira amesema mazingira ya eneo la Pasua Block JJJ ni tofauti na maeneo mengine yaliyowekewa alama X wakitakiwa wabomoe kwa kuingilia hifadhi ya reli.


“Kama Reli ilibadilisha matumizi ikasema eneo ligawanywe basi limegawanywa kimakosa. Tayari nimemwambia mkurugenzi (wa Manispaa) wafanye mazungumzo na Rahco wawape eneo lingine,”amesema Mghwira.


Mghwira amesema njia hiyo ndio pekee inayoweza kuepusha wananchi waliopewa viwanja kihalali na Halmashauri kuvunjiwa nyumba zao lakini akasisitiza wale waliopo ndani ya hifadhi ni lazima wabomoe nyumba zao.


Wananchi wote wa eneo hilo wanazo nyaraka halali zilizotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kuanzia barua ya toleo, hati miliki, vibali vya ujenzi na nyaraka za malipo ya kodi mbalimbali za Serikali.


Mkazi wa eneo hilo, Japhet Mmbaga, alimuomba Rais Magufuli kuingilia kati suala hilo akisema analifahamu vizuri na kwamba mchakato wa utwaaji wake ulikuwa na baraka zake akiwa waziri wa Ardhi.


“Watu watofautishe hili jambo. Kuna watu wamevamia maeneo ya reli na wengine wako ndani ya mita 30. Sisi ni tofauti eneo hili lilitwaliwa na Halmashauri kwa taratibu zao ndio wakaligawa,”amesema.


“Rais Magufuli akiwa Waziri wa Ardhi alishakuja hapa Moshi kwa suala hili kwa hiyo analijua vizuri. Waziri Mkuu Pinda (Mizengo) naye alishakuja kwa hiyo ni suala linajulikana kwa mamlaka,”amesisitiza.


Mmbaga amesema wao kama watanzania, hawapingi maendeleo lakini kama Serikali inaona kuna haja ya kurudisha lengo lile la miaka ya 60, basi haina budi kuwafidia kwa vile waligawiwa kihalali.


Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya, amesema walioweka alama hizo wamekosea na anaamini Serikali itatoa ufafanuzi na kusitisha ubomoaji katika eneo hilo la Pasua lililogawiwa kihalali.