Monday 25 September 2017

Mbunge CHADEMA amesema ana ushahidi usiotia shaka



Mbunge Arumeru Mashariki (CHADEMA), Joshua Nassari amefunguka na kusema yeye ana ushahidi usiotia shaka juu ya madiwani ambao wamepokelewa jana na Rais kuwa wamenunuliwa na kupewa rushwa na si kuwa wamehama kwa lengo la kukubali kazi anazofanya Rais 


Nassari amesema hayo leo jijini Arusha alipokuwa akiongea na waandishi wa habari na kusema yupo tayari kukutana na Rais Magufuli, IGP Sirro, Mkurugenzi wa TAKUKURU, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kuwaonyesha ushahidi huo na kama wateule wa Rais wa Mkoa wa Arusha watakataa juu ya ushahidi huo basi yeye yupo tayari kujiuzulu Ubunge wake. 


"Kuondoka kwa hawa madiwani ni rushwa ya mfumo kupitia wateule wa Rais aliyewateua yeye waliopo hapa Arusha, kwa wakati wowote atakapohitaji nipo tayari kumuonyesha, tulikuwa tunajua nini kinaendelea na biashara hii imefanyika kwenye ofisi za umma yaani ofisi za serikali, na huo ushahidi nilionao nimeufanyia kazi kwenye ofisi za Umma kwa hiyo vyombo vya usalama vitakavyokuwa tayari nitavionyesha ushahidi huu pasipokuwa na shaka yoyote, endapo ushahidi huu utakuwa si wa kweli kwamba hawa watu hawajanunuliwa nipo tayari kujiuzulu ubunge wangu" alisema Nassari 


Aidha Nassari amesema kuwa madiwani hao ambao wamehama kutoka CHADEMA na kwenda CCM na kupokelewa jana wamepewa mpaka ulinzi na serikali 


"Watu hao wamepewa mbaka ulinzi wabunge tumelia Dodoma Mbunge mwenzetu Tundu Lissu amepigwa risasi lakini kabla ya kupigwa risasi alikuwa analalamika na kupiga kelele kuna watu wanamfuatilia akataja mpaka namba za gari lakini hakupewa ulinzi wowote, hapa Arusha diwani anahama halafu anapewa ulinzi na vyombo vya usalama, wateule wa Rais wanamuhakikishia ulinzi na usalama, lakini yupo Mbunge ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa kambi mbaka anakuja kupigwa risasi hajapewa ulinzi wa aina yoyote anaambiwa hakutoa taarifa" alisema Nassari 


Nassari alimalizia kwa kusema madiwani hao mbalimbali ambao wameondoka CHADEMA na kuhamia CCM wamenunuliwa kwa kupewa rushwa na wateule wa Rais na kwamba kusema wamekwenda huko kwa kuwa wamekubali utendaji wa serikali ya awamu ya tano si ukweli.