Saturday 12 July 2014

UMECHOSHWA NA UPWEKE? JARIBU KUZINGATIA HAYA

Nimatumaini yangu kwamba msomaji wangu na rafiki yangu uko poa! Karibu
tena katika busati la mahaba, mahali ambapo tunabadilishana mawazo,
kujuzana na kushauriana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo mapenzi.Wiki
iliyopita nilianza kueleza kuhusu mada hiyo hapo juu ambayo ilikuwa

maalum kwako wewe rafiki yangu ambaye umri wa kuoa umefika lakini
unasumbuliwa na upweke na hujui jinsi ya kumnasa mwanamke au mwanaume
wa maisha yako.Nilikufafanulia namna ya kumsogeza karibu mtu
unayempenda kwa njia ya simu kama unaogopa kumwambia ana kwa ana
ambapo hatua ya kwanza tulisema ni kupata namba yake ya simu kisha
baada ya hapo kuanza kujenga naye mazoea taratibu, ukimtumia meseji
nzuri mara kwa mara.Rafiki, baada ya kuupata ukaribu wake, jaribu kuwa
unamsifia mara kwa mara. Akiwa amekolea na sifa unazomwagia, mweleze
kwamba unavutiwa naye na unatamani kuwa na mpenzi anayefanana
naye.Zungumza naye kwamba atakapokubali kuwa na wewe, utamtunza,
kumheshimu na kumlea kama malkia au mfalme, mweleze malengo yako ya
baadaye katika uhusiano wenu endapo atakukubalia.Usimpe nafasi ya
kukwambia kama amekubali au amekataa bali hitimisha mazungumzo yenukwa
kumtakia siku njema au kazi njema. Bila shaka utamuacha akiwa na
shauku kubwa ya kuendelea kusikiliza 'mistari' yako.Endelea
kuwasiliana naye kwa mambo ya kawaida huku ukimpima kama yale
uliyomwambia anayachukuliaje. Kama naye amekupenda, utaanza kuona
mabadiliko kuanzia meseji atakazokuwa anakutumia, namna anavyopokea
simu yako na uchangamfu anaokuonesha.Kama bado haoneshi dalili zozote
za kukuelewa, basi jua hajavutiwa na wewe na ukiendelea kuzungumzia
mambo ya mapenzi, huenda ukaanza kum-boa lakini kama ana dalili za
kuingia kwenye kumi na nane zako, endeleza mawasiliano naye, omba
kukutana naye sehemu tulivu kama ufukweni au popote ambapo mtakuwa
wawili na hapo utakuwa na nafasi nzuri ya kueleza kwa kina juu ya
hisia zako.Endapo atakubali kukutana na wewe, basi hiyoni hatua nzuri
sana kuonesha kwamba unaelekea kufanikiwa. Jambo la msingi ni kuanza
kujiandaa kwa ajili ya kukutana naye kwa sababu mwonekano wako wa
kwanza mbele ya macho yake ndiyo utakaompa sababu ya kukuchagua au
kukukataa.Kwanza anza kwa kufanya kitu ambacho huwa kinakufurahisha na
kukuweka kwenye mudi nzuri kama kuimba, kucheza muziki, kufanya
mazoezi au chochote unachokipenda sana.Baada ya hapo, hakikisha nguo
zako ni safi, jipulizie manukato mazuri, piga mswaki, jitengeneze
nywele zako
vizuri na hakikisha kila kitu mwilini mwako ni
kisafi.Pangilia mazungumzo kati yako na umpendaye kabla hata
hamjakutana, hii itakuongezea kujiamini.Hakikisha sehemu mnayoenda
kukutania kwa mara ya kwanza unaifahamu vizuri na imetulia vya
kutosha.Baada ya hapo, muandalie zawadi ndogo mfano chokleti, mkufu au
ua zuri. Usihangaike kutafuta zawadi kubwa kwa sababu siyo muhimu
mnapokutana kwa mara ya kwanza.Muda utakapowadia, wahi kufika eneo
mlilopanga kabla ya mwenzako, hii itamfanya akuheshimu zaidi kwa
sababu atajua hubahatishi mambo.Msalimie kwa uchangamfu kisha
mkaribishe sehemu ya kukaa. Jitahidi kupunguza manenomengi badala yake
zungumza kwa staha na muda mwingi msikilize yeye. Muulize kinywaji au
chakula anachokipenda kisha muagizie.Kama wewe ni mwanaume,
mkishamaliza kunywa au kula, lipa bili hata kama yeye anao uwezo wa
kulipa. Ukweli ambao wengi hawaujui, wanawake wanapenda zaidi
kuhudumiwa hata kama wana utajiri mkubwa kiasi gani.Mkishamaliza,
uwanja ni wako sasa wa kueleza hisia za ndani ya
moyo wako.Zungumza
kwa busara na kwa utulivu, huna haja ya kupaniki kwa sababu mpaka
amekubalikukutana na wewe, tayari una asilimia kubwa ya kumpata hivyo
punguza woga. Jitahidi kumtazama kwenye macho yake unapozungumza naye,
hii itakuongezea ujasiri.Naam! Baada ya hapo naamini utakuwa umeutua
mzigo mzito uliokuwa nao, usimlazimishe kukupa majibu hapohapo endapo
ataomba umpe muda.Baada ya hapo, tayari utakuwa umefanikiwa kumvuta
kwako kwa asilimia tisini, ongeza ukaribu zaidi na utaona matokeo yake
kwa sababu hataweza kukataa ombi lako na mwisho mtatimiza lengo lenu
la kufunga ndoa na kuishi pamoja siku za mbele.