Monday 23 October 2017

Waziri Tillerson asema wanamgambo wa Shia Iraq 'warudi nyumbani'

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amewaambia wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq warudi nyumbani wakati vita dhidi ya kundi la Islamic State vinamalizika.
Alitoa matamshi hayo wakati wa ziara Saudi Arabia na Qatar, iliyolenga kujaribu kusitisha ushawishi wa Iran katika eneo hilo.

Lakini alishindwa kupiga hatua katika kutatua mzozo mkali baina ya washirika hao wa Marekani.
Marekani ina wasiwasi kwamba Iran itapatiliza hatua zilizopigwa dhidi ya Islamic State nchini Iraq na Syria kupanua ushawishi wake katika nchi hizo.

Nchini Iraq, wapiganaji wa madhehebu ya Shia wanaoungwa mkono na Iran wameshiriki katika vita hivyo, lakini Rex Tillerson amesema sasa muda umewadia kwao ima kujumuika katika jeshi la Iraq au warudi nyumbani.

Alijadili pia sera yao mpya na Saudia dhidi ya Iran akionya kuwa makampuni ya Ulaya yanayoendesha biashara na Iran, wanafanya hivyo wakiwa katika hatari kubwa, kutokana na vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran.

Wakati huo huo waziri huyo amekiri kwamba huenda Iran ikatumia mzozo kati ya washiriki wa Marekani wa madhehebu ya Sunni: mataifa manne yanayoongozwa na Saudia yalioishutumu Qatar kwa kuunga mkono wapinzani wa serikali na kuidhinisha marufuku.

Lakini amesema licha ya jitihada, Saudia haiko tayari kuidhinisha mazungumzo ya moja kwa moja na Qatar katika kuutatua mzozo.