Tuesday 24 October 2017

Rais Magufuli shikilia hapo hapo – Prof. Lipumba

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof Ibrahim Lipumba amesema anaunga mkono juhudi zinazofaywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli za kusimamia rasilimali za Watanzania.

Prof. Ibrahim Lipumba na Rais, John P. Magufuli

Prof Lipumba amesema juhudi anazozifanya Rais Magufuli ni lazima ziungwe mkono na kila mtu kwani zina lengo la kuokoa rasilimali zetu na zina manufaa kwa Watanzania.

“Naomba kumpongeza Rais ‘Magufuli’ kwa juhudi alizozifanya katika suala hili la madini, sisi viongozi wa vyamasiasa hususani vya upinzani kwa muda mrefu , kwa miaka mingihasa tokea mwaka 2000 tumekuwa tukipiga kelele sana kuhusu mikataba ya madini na namna rasilimali zetu zinavyoibiwa, tunakupongeza Rais kwa sababu jambo hili umelichukulia umuhimu unaohitajika kuweza kuleta mabadiliko, itakuwa ajabu sisi tuliokuwa mstari wa mbele kupiga kelele kuwa tunaibiwa tuweze kubeza juhudi ambazo umezifanya.“amesema Prof Lipumba leo Ikulu jijini Dar es salaam kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa kamati iliyofanya tathmini ya thamani ya makinikia na madini, Hafla iliyoongozwa na Rais Magufuli.

Hata hivyo, Prof. Lipumba amemuomba Rais Magufuli aendelee kuongeza juhudi za uokoaji wa rasilimali “Rais nakupongeza sana endelea kushikilia hapo hapo, na Palamagamba endelea na kazi na shikilia msimamo huo huo, rasilimali za nchi yetu ziweze kulindwa.“