Wednesday 25 October 2017

Mabalozi wainyooshea kidole Kenya

Nairobi, Kenya. Mabalozi wa nchi za Ulaya na Marekani wamezungumzia “kuzorota kwa mazingira ya kisiasa” katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa marudio na wakahimiza vyama vikuu kujizuia kufanya uchochezi na kuacha kuzikashfu taasisi.

Balozi wa Marekani nchini Kenya Robert Godec aliyezungumza kwa niaba ya mabalozi wengine amesema ikiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) itahisi kuwa haiko tayari kwa uchaguzi wa Alhamisi basi iombe ridhaa mahakamani usogezwe mbele.

Godec alisema hayo jana alipokuwa anasoma taarifa ya wanadiplomasia 20 kutoka nchi za Magharibi wakiwemo wa Umoja wa Ulaya wenye wanachama 28, wakitoa wito wanasiasa hasimu kuungana ili kuwezesha uchaguzi wa kuaminika kufanyika baada ya wiki kadhaa za matukio yanayokanganya na kuligawa taifa.

Wakenya, Alhamisi watakwenda kwenye vituo kupiga kura katika uchaguzi wa marudio baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta ikitaja kuwepo dosari na kukoasa uhalali.

Soma: Wakenya watakiwa kudumisha amani na utulivu

Uamuzi huo nadra uliompa ushindi mlalamikaji kiongozi wa upinzani wa Nasa, Raila Odinga, ambaye sasa amesusa kushiriki uchaguzi wa marudio, amekuwa akiishutumu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kushindwa kufanyia marekebisho muhimu.

Raila ameitisha mgomo siku ya uchaguzi na aliandikwa kwenye Twitter akiwataka wafuasi wake kuweka vigini kwenye ofisi za IEBC leo na kesho.

Wanadiplomasia hao wamelaani matukio hayo ambapo maofisa wa uchaguzi wamekuwa wakishambuliwa na pia kuvurugwa kwa maandamano madarasa ya mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi.

"Mashambulizi dhidi ya maofisa wa IEBC lazima yakomeshwe. Hakuna anayelazimishwa kugombea au kupiga kura ikiwa haoni haja hiyo,” alisema Godec.

"Lakini vurugu zisitumike au vitisho kuvuruga haki ya wengine kupiga kura au kushiriki. Kufanya hivyo si vitendo vya kidemokrasia na viongozi lazima wawambie wafuasi wao kujiuzuia kufanya vitendo viovu.”