Monday 23 October 2017

Tatizo la Kichefuchefu kwa wanawake zaidi

Watu wengi wanaume kwa wanawake, husumbuliwa na matatizo ya ulaji yanayoathiri afya na mfumo wa maisha yao ya kila siku.

Moja ya matatizo yanayohusiana na ulaji ni tatizo la muda mrefu la kichefuchefu,
kinyaa, kukosa hamu ya chakula na kutapika hasa kwa wanawake.

Kichefuchefu ni ile hali ya mtu kujikuta katika mazingira ya hisia zinazochochea tamaa ya kutapika kwa lengo la kuondoa kile kilichopo tumboni.

Hali hiyo huandamana na mate mdomoni kubadilika na kuwa mepesi na mengi kiasi kwamba hujihisi kutaka kuyatema mara kwa mara na hujikuta anatapika iwapo atalazimisha kuyameza.
Kimsingi kuna magonjwa mengi yanayosababisha kichefuchefu na kutapika ambayo yanaweza kuwapata wanawake.

Magonjwa haya ni kama vile minyoo, maambukizi ya bakteria katika njia ya mkojo, ugonjwa wa kisukari, matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi zake vizuri, homa ya ini, ugonjwa wa kuvimba kwa kidole tumbo na vidonda vya tumbo.

Matatizo mengine ni pamoja na kujifunga kwa utumbo, matatizo ya kujinyonganyonga na kujifunga kwa vifuko vya mayai na ujauzito.

Tatizo la kukosa hamu ya chakula na kichefuchefu pia linaweza kuwapata wasafiri wa baharini, wagonjwa wanaotumia dawa kali, watumiaji wa mihadarati, walevi wa kupindukia na pengine hata wanaokutana na harufu mbaya na kali kushinda uwezo wa kuimudu.

Wengine ni wale wanaougua magonjwa ya mchafuko wa tumbo unaotokana na kuharisha, kipindupindu, homa ya malaria, dengue au ebola.

Kwa wasichana wengi matatizo ya kisaikolojia huchangia kuamsha hali ya kichefuchefu inayosababisha kutotamani baadhi ya vyakula au kutopenda aina fulani za harufu.

Matatizo haya mara nyingi hutokea katika kipindi cha utoto na usichana na yanaweza kutokea katika kipindi cha utu uzima pia.

Matatizo haya ya kisaikolojia yanaweza kusababisha mtu achukie chakula na kula kiasi kidogo sana au kupata kinyaa, kichefuchefu na kutapika mara kwa mara.
atizo hili la kisaikolojia mara nyingine humfanya mtu kuchunguza sana chakula, tunda au kinywaji kabla ya kukila.

Pale anapoona dalili za hisia au kuona kitu hicho kuwa na chochote asichokipenda hukiacha au kama atakuwa tayari amekula huanza kupata kichefuchefu na kutamani atapike.

Watu wa namna hiyo mara nyingine hujikuta wanakuwa waangalifu sana katika kula kwa mfano kama anakula andazi, ataondoa ngozi ngumu ya nje kwa vile ipo katika mwonekano wa kuwa na hali ya mafuta na kuhakikisha anakula tu kile kilichopo ndani. Huyu kichefuchefu chake kinakuwa kinachochewa na mafuta au nyama yenye mafuta.

Moja ya sababu zinazochangia kutokea kwa tatizo hili hasa kwa wasichana ni ile hali ya kuona kinyaa.
Wakati mwingine husababishwa na hali ya kuogopa sana unene kutokana na mtazamo kuwa wasichana wembamba ni wazuri na wanaopendeza zaidi.

Kutokana na kutawaliwa na mawazo hayo, wasichana wengi hujizuia kula ili kupunguza unene na uzito kiasi kwamba hupata athari za kiafya.

Tatizo hili kitabibu hujulikana kama ‘anorexia nervosa’ ambalo moja ya dalili zake ni pamoja na kichefuchefu.
Kwa mujibu wa Don Hockenbury na Sandra Hockenbury katika kitabu chao kiitwacho ‘Psychology’ kilichochapishwa mwaka 2008, hali hii huwapata wanawake takribani mara tisa zaidi ya wanaume.

Mnamo mwaka 2005, tovuti ya cureresearch.com katika ufuatiliaji wa tatizo hili, ilitoa taarifa kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapatao 36,070 wa tatizo la anorexia nervosa.

Katika utafiti uliowahusisha wasichana 214 wa Kitanzania, ilibainika kuwa theluthi moja kati ya hao walikuwa na matatizo yanayohusu ulaji kama vile kichefuchefu, kukosa hamu ya chakula na kutapika mara kwa mara.

Pia matatizo haya yalionyesha uhusiano wa karibu na mila za kimagharibi kutokana na kusafiri ng’ambo au kupata habari za huko kupitia vyombo mbalimbali vya mawasiliano na matangazo ya biashara yanayohusiana na urembo.

Utafiti huo ulifanywa na Eddy KT wa Kitivo cha Saikolojia cha Chuo Kikuu cha Boston kwa kushirikiana na Hennessey M pamoja na Thompson-Brenner H na kuchapishwa katika jarida la magonjwa ya akili toleo la 195(3) la Machi 2007.

Katika utafiti mwingine uliofanyika huko Ghana maeneo ya vijijini ukiwahusisha wasichana 668 wa shule za sekondari, jopo la watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh ulibaini kuwa tatizo hili lipo hapa Afrika na halitokani na kuiga maisha ya kimagharibi pekee.

Dk Alan Carson, daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh, anasema haionyeshi wazi kuwa hili linatokana na kuiga mila na kigeni.

Hata hivyo, utafiti huo ulibaini kuwa zaidi ya nusu ya wasichana walioshiriki katika utafiti huo waliwazia sana hali ya mwonekano wao na theluthi mbili walijiona kuwa hawapendezi wanapojilinganisha na wanawake wazuri wanaoonyeshwa na vyombo vya habari vya nchi za magharibi katika matangazo ya urembo.

Asilimia 88 ya wasichana wote walikiri kuwa wanajisikia kushinikizwa na matangazo ya urembo kuhusu mwonekano wa uzuri wa umbo la msichana.

Utafiti mwingine uliofanyika Sweden ukihusisha zaidi ya pacha 31,400 ulikadiria kuwa asilimia 56 ya mwelekeo wa mtu kupata ugonjwa wa kisaikolojia unasababisha kichefuchefu na kukosa hamu ya chakula, unatokana na urithi wa kijenetiki.

“Asilimia 56 ya urithi – hicho ni kiwango kikubwa kinachotokana na urithi wa vinasaba,” anasema Cynthia Bulik, kiongozi wa utafiti huo uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Archives of General Psychiatry la mwezi Machi 2006.

Blogu ya fashionnewstanzania.blogspot.com mnamo April 2012, ilitoa orodha ndefu ya wanamitindo wa nchi mbalimbali duniani waliofariki katika karne ya 21 na miongoni mwa sababu za vifo vyao ni tatizo la anorexia nevosa.

Orodha inayofanana na hiyo pia imetolewa na kamusi elezi ya Wikipedia kupitia tovuti yao ya en.wikipedia.org ya Agosti 17, 2014.

Katika utafiti wake uliochapishwa mwaka 2008 katika jarida lake la Child and Adolescent Psychiatric Clinics of North America, Steinhausen HC alibainisha kuwa watu wenye tatizo hili wana uwezekano wa kufa mapema mara 18 zaidi ya wenzao wenye umri sawa katika jamii.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa watu wenye tatizo hili la afya ya saikolojia hukabiliwa na ukondefu mkubwa kuliko kawaida, utapiamlo unaotokana na kula kiasi kidogo sana cha chakula na kutokupata damu ya hedhi kama kawaida kwa wasichana na wanawake.

Watu wenye tatizo hili pia wanakuwa na athari za kisaikolojia hujiona kuwa bado ni wanene hata pale mwili wao unapokuwa umepungukiwa na uzito kwa kiasi cha kudhuru afya.

Watu hawa hulazimika kujipima uzito mara kwa mara, kubagua vyakula, kunywa maji ya moto, kufanya mazoezi mazito ya mwili na wakati mwingine hujilazimisha kutapika au kutumia dawa zinazosababisha kuharisha na kukojoa sana.

Kutokana na sababu hizo wengi hupata shida ya kushuka kwa msukumo wa damu ama kwa namna nyingine shinikizo la chini la damu.

Matatizo mengine ni upungufu wa damu kwa kiasi fulani, kukauka kwa ngozi, nywele na kucha hupoteza afya yake ya asili kiasi kwamba hulazimika kutumia rangi za kucha na vipodozi mbalimbali ili kujiremba.

Matatizo mengine yanayowapata watu wenye tatizo hili ni pamoja na haja kubwa kuwa kavu sana kunakosababishwa pia na kukosa choo muda mrefu, uchovu wa mwili, kushindwa kupata watoto na matatizo ya moyo na ubongo ya kutokufanya kazi vizuri.

Hali hii mara nyingi husababishwa na kuparaganyika kwa utendaji mwili hasa kwa kemikali zilizopo mwilini.

Kichefuchefu huweza kumwathiri mtu kisaikolojia kiasi kwamba kama ni mwanafunzi darasani, msafiri ama kwenye mkutano huweza kumfanya mtu asiweze kutulizana.
Mara kwa mara atapenda kutema mate na hali hii inaweza pia kumfanya atapike kwenye hadhira ya watu.

Ni vizuri mtu akajijua juu ya hali ya afya yake na akapata ushauri mapema ili isiwe ni kizuizi cha kutekeleza mipango yake.

Hospitali nyingi nchini zinao wataalamu wa sayansi ya tiba wanaoweza kutibu kwa ufanisi tatizo hili.