Monday 23 October 2017

Kylian Mbappe atwaa tuzo ya Golden Boy

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa na klabu ya Paris Saint-Germain inayoshiriki ligi One ya nchi hiyo, Kylian Mbappe ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka mwenye umri mdogo barani Ulaya inayojulikana kama (Golden Boy award ) na kuwazidi wachezaji, Gabriel Jesus wa Manchester City na Ousmane Dembele wa FC Barcelona.


Mbappe mwenye umri wa miaka 18, ameanza kufahamika zaidi msimu uliyopita baada ya kufunga mabao sita katika michuano ya klabu bingwa barani Ulaya akiwa na klabu ya Monaco na kuisaidia kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.

Kylian Mbappe ameiwezesha Monaco kuchukua ubingwa wa ligi One huku akifunga mabao 15, kwa sasa mchezaji huyo amekwenda klabu ya PSG kwa mkopo ambapo ameshatupia mabao manne na kutoa pasi 11 zilizochangia mabao.

Mchezaji huyo atasajiliwa rasmi na PSG kwa dau la paundi milioni 166 msimu ujao wa majira ya joto.

Mbappe ameshinda tuzo hiyo kwa jumla ya kura 291 wakati mchezaji wa Barcelona, Dembele akishika nafasi ya pili kwa kuwa na kura 149 huku kijana wa meneja Pep Guardiola wa Man City, Gabriel Jesus akishika nafasi ya tatu wakati nafasi ya nne ikishikwa na Marcus Rashford wa Manchester United.

Tuzo hiyo inayoendeshwa na Tuttosport ni mwaka wa 15 sasa inatolewa wakati wachezaji kama Wayne Rooney, Mario Balotelli, Raheem Sterling na Anthony Martial walishawahi kuinyakuwa.