Sunday 14 May 2017

FAHAMU Njia 16 za Kuondoa Sumu Mbalimbali Mwilini...!!!

Mwili unaweza kupatwa na sumu au takataka zisizohitajika na mwili kwa namna mbili, ama kupitia mazingira tunayoishi (viwanda, migodi nk) au kupitia vyakula na vinywaji ambavyo tunatumia kila siku. Sumu au taka pia zinaweza kuingia mwilini kupitia dawa mbalimbali hasa za kizungu tunazotumia kujitibia magonjwa mbalimbali.


Mwili huzalisha hizi sumu au takataka (free radicals) kila mara kunapofanyika mmeng’enyo wa chakula mwilini mwako.


Njia 16 za kuondoa sumu mbalimbali mwilini


1. Fanya mlo wako mmoja wa siku kuwa ni matunda pekee


Amua moja ya mlo wako kwa siku uwe ni matunda pekee bila chakula kingine zaidi. Unaweza kuamua ama chakula cha asubuhi au cha jioni kuwa ni matunda pekee, ndiyo kwenye sahani yako unajaza matunda tu mbalimbali sahani ijae na ule hayo tu kama ndiyo mlo wako ukimaliza unaweza kunywa juisi ya matunda au maji pekee.


2. Kula vyakula vya asili zaidi kuliko vya viwandani


Kama unataka kuepuka sumu au takataka nyingine kirahisi kuingia katika mwili wako basi pendelea zaidi kula vyakula vya asili vinavyopikwa nyumbani kuliko kula vya kwenye makopo au vya dukani au vya kwenye migahawa (fast foods).


3. Fanya masaji


Kwa bahati mbaya waTanzania wengi hawajuwi kuwa masaji ni sehemu ya tiba au ni dawa pia kwa magonjwa mengine mengi mwilini. Wengi tunaichukulia masaji kama kitu cha starehe tu (relaxation) lakini unaweza kutumia masaji kama njia mojawapo ya kuondoa sumu mwilini na utafanikiwa kwa muda mfupi sana.


4. Kunywa maji mengi kila siku


Sababu kubwa ya watu wengi kutengeneza sumu au taka mwilini mwao ni kutokunywa maji mengi kila siku. Maji ni uhai, bila kunywa maji mengi kila siku ni sawa na kwenda dukani bila hela mfukoni. Haijalishi upo mazingira gani kama ni ya baridi au ni ya joto ni LAZIMA UNYWE MAJI YA KUTOSHA KILA SIKU IENDAYO KWA MUNGU.


Unahitaji maji glasi 8 mpaka 10 kila siku. Watu wengi wanahangaika namna ya kuondoa sumu kusafisha miili yao bila kujua kuwa maji pekee ya kunywa yanatosha kwa kazi hiyo. Kumbuka asilimia 94 ya damu yako ni maji, asilimia 85 za ubongo wako ni maji, hivyo ili kusafisha damu na mwili kwa ujumla ni lazima unywe maji ya kutosha kila siku.


5. Acha chai ya rangi na Kahawa


Kama tayari imethibitika una sumu au takataka nyingi mwilini nakushauri uache kunywa chai ya rangi na kahawa. Badala yake hamia kutumia chai yenye tangawizi au mdalasini au mchaichai. Chai ya rangi na kahawa vina kaffeina ambayo kwanza huyasukuma maji nje ya mwili kwa haraka na kuuacha mwili bila kuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kazi zake. Kaffeina pia ni madawa ya kulevya kundi la madawa yanayosisimua mwili (stimulants drugs).


6. Fanya mazoezi ya viungo


Inashangaza sana kuona waTanzania wengi hawaoni umhimu wa kufanya mazoezi ya viungo. Mazoezi ya viungo ni jambo la lazima kama ilivyo chakula. Iwe unaumwa au huumwi, iwe una uzito kuzidi au una uzito wa kawaida hakikisha unapata muda wa kufanya mazoezi.


Mazoezi yanakusaidia kukufanya ujisikie vizuri na hivyo kukuondolea mfadhaiko au stress kirahisi zaidi, sambamba na hilo mazoezi ni dawa tosha na nzuri ya kuondoa sumu mwilini haraka zaidi. Hakikisha jasho linakutoka la kutosha na iwe ni jambo la kila mara na siyo unaenda jumamosi na jumapili (weekend) tu, hiyo haitoshi, fanya mazoezi mara 4 mpaka mara 5 kwa wiki.


7. Kula zaidi vyakula vyenye nyuzinyuzi (faiba)


Umesikia mara nyingi kwamba unahitaji kula zaidi vyakula vyenye nyuzinyuzi kwa ajili ya kuwa na afya bora, mmeng’enyo wa chakula wenye afya na hata kukusaidia kupunguza uzito. Kile ulikuwa hujuwi pengine mpaka sasa ni kuwa vyakula hivi vyenye nyuzinyuzi ni vizuri pia katika kusafisha mwili na kuondoa sumu au takataka mbalimbali.


Vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi ni pamoja na parachichi, ndizi, peazi, karoti, pilipili hoho, mchele wa brown (ule wanashauriwa watu wa kisukari wautumie), maharage meusi, njegele, tende, viazi vitamu, tufaa (apple), machungwa, ugali wa dona pia mkate wa unga wa ngano ambao haujakobolewa.


8. Funga kula


Ndiyo, kama ulikuwa hujuwi namna nyingine rahisi ya kuondoa au kupunguza sumu mwilini ni kufunga kula kabisa kutwa nzima. Ukifunga kula mwili unalazimika kuvitumia vile vilivyomo ndani yake bila kushughulika kuvisaga vingine vipya unavyokula. Kunapokuwa hakuna shughuli ya kuvisaga na kumeng’enya chakula kipya mwilini ndipo mwili unaweza kuondoa sumu na taka nyingine kirahisi zaidi.


Amua kufunga kula kabisa kwa wiki mara 2 hata 3 ili kuondoa au kupunguza sumu, hii inaweza kuwa pia ni njia mojawapo ya kufanya maombi na kujiweka karibu na muumba wako.


9. Pata usingizi wa kutosha kila siku


Moja ya vitu vinaweza kukupelekea kuwa na sumu mwilini au takataka nyingi ni pamoja na kutokulala muda wa kutosha kila siku. Usingizi haukopwi na huwezi kuwa na ufanisi katika kazi zako kama hupati usingizi wa kutosha kila siku.


Usingizi siyo jambo la starehe tu, ni sehemu mhimu sana katika afya yako ya kila siku. Bila kupata usingizi wa kutosha unaweza kuwa karibu na matatizo kama kuongezeka uzito, kushuka kwa kinga ya mwili na nguvu zako za mwili kwa zinaweza kushuka.


Unapopata muda wa kutosha wa kulala masaa 7 mpaka 8 kwa siku unaupa mwili wako nafasi ya kutosha ya kupumzika na kujiripea upya na hivyo ndivyo sumu na takataka nyingine zinavyoweza kukutoka kirahisi. Ingia kulala mapema walau saa tatu usiku ingia kulala siyo unakaa unaangalia tamthiliya au mpira mpaka saa sita za usiku!


10. Epuka mazingira hatarishi kwa sumu


Kuna mazingira yanajulikana wazi kuwa ni vyanzo vya sumu mwilini. Maeneo ya migodi ya madini, maeneo yenye viwanda vingi, maduka yanayouza dawa za kilimo nk


Maeneo haya yanafaa kukaa mbali na makazi ya binadamu kwa usalama wa afya zetu.


11. Tumia mtindi


Moja ya njia nyingine ya kuondoa sumu na takataka nyingine ni kutumia vyakula vyenye bakteria wazuri (probiotics). Mtindi ndicho chakula pekee kinajulikana kuwa na bakteria hawa wazuri kwa ajili ya tumbo lako. Pata mtindi kikombe kimoja kila siku na utabaki na mwili msafi muda wote. TUmia mtindi wa nyumbani ndiyo mzuri zaidi ingawa hata wa dukani nakuruhusu utumie hasa ule ambao haujaongezwa kingine chochote ndani yake (flavors and additives).


12. Epuka vyakula vilivyokobolewa


Ili kuwa na mwili msafi kabisa epuka kula mkate mweupe, sukari na vyakula vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi kama vile chipsi, maandazi na vingine vyote vinavyochomwa katikati ya mafuta mengi.


Mkate upo mkate mweusi (brown bread), sukari ipo asali mbichi, vyakula vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi unaweza kuamua kuwa unavioka (bake) au uvichemshe (boiling). Uchaguzi ni wako.


13. Ondoa mfadhaiko (stress)


Kile tayari unajuwa ni kuwa mfadhaiko au stress ni jambo baya kwa afya yako. Kile unatakiwa kujua kuanzia sasa ni kuwa ili kubaki na afya bora kabisa yenye TBS basi ukae mbali na stress. Kama utaruhusu stress kutawala maisha yako basi ujuwe mwili wako hauwezi kufanya kazi zake vizuri ikiwemo ya kuondoa taka au sumu mbalimbali mwilini.


Stress peke yake inaweza kupelekea magonjwa mbalimbali mwilini zaidi ya 50. Unapokuwa na mfadhaiko mwili wako hauwezi kutoa taka nje kirahisi na kinga yako ya mwili inashuka matokeo yake unakuwa karibu na magonjwa mengine mengi.


Watu wengine wenye uelewa mdogo wakiwa na stress hukimbilia kutumia vilevi wakidhani zitapungua kumbe ndiyo wanazidi kuongeza tatizo bila kujua. Vitu viwili vinaondoa stress bila kulazimika kutumia njia mbaya kwa afya yako ni mazoezi ya viungo na tendo la ndoa. Siku nyingine ukijiona umefadhaishwa sana nenda kafanye mazoezi ya kufa mtu ikiwezekana baadaye tafuta mtu shiriki tendo la ndoa.


14. Tumia dawa za asili badala ya zile za kizungu


Dawa nyingi za hospitali huwa zina matokeo chanya (positive) na matokeo hasi (negative) pia ambayo ndiyo matokeo mabaya. Kama unalazimika kutumia antibiotic kila mara au unameza dawa za kuondoa maumivu kila mara unaweza kuwa unaongeza sumu na taka mwilini bila kujua na bila sababu yoyote ya lazima.


Kuepuka hilo jaribu kutumia mitishamba au mimea ya asili kwa baadhi ya magonjwa ambayo si lazima uende hospitali. Siyo mafua tu mtu ameenda kuchoma sindano!


15. Acha vilevi


Moja ya vitu vinavyoweza kuleta sumu au taka mwilini moja kwa moja ni vilevi. Vilevi kama pombe, madawa ya kulevya, sigara, bangi na vinginevyo ni vitu vinavyopelekea mwili kuwa na taka moja kwa moja.


Namna pekee ya kuondoa sumu kutokana na vilevi ni kuviacha hivyo vilevi, ndiyo kuviacha. Usitegemee asubuhi utumie dawa kuondoa sumu mwilini halafu jioni ukanywe pombe au ukavute sigara utegemee tu ile dawa uliyotumia asubuhi kwamba itafanya kazi, hapana unajidanganya, dawa ni kuacha vilevi moja kwa moja.


Vingine vya kuacha kama tayari imegundulika una sumu nyingi mwilini ni pamoja na vinywaji baridi vyote, juisi zote za dukani, chai ya rangi na kahawa.


16. Tumia vifuatavyo kuondoa sumu zaidi


Vifuatavyo vinaondoa sumu kirahisi zaidi mwilini; kitunguu swaumu, unga wa majani ya mlonge na mbegu zake na mbegu za maboga au unga wake. Kitunguu swaumu Mlonge Mbegu za maboga