Tuesday 30 May 2017

Gwajima amvulia kofia Magufuli

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ameonesha kufurahishwa na maamuzi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kitendo cha kusimamisha makontena ya kusafirisha mchanga wa dhahabu wiki iliyopita na kusema kuwa hiyo ni hatua ya ukombozi wa maliasili za taifa.


Askofu, Josephat Gwajima

Mchungaji Gwajima amesema Tanzania ina vitu na mali nyingi sana ila vimetelekezwa kwa wazungu na kuiacha nchi ikiwa masikini tena kwa tamaa ndogo ndogo kwa baadhi ya viongozi hivyo amemsihi Rais Magufuli kushikilia hapo hapo kwenye makontena mpaka kieleweke.

“Hata kama tulisaini mikataba ya kufa mtu sawa tu Rais ashikirie hapo hapo hakuna kuruhusu makontena mpaka wazungu macho yao yawe mekundu, kama hatujawa tayari kuchimba madini tuyaache kwanza, wapo wanaosema sijui tutashitakiwa, sijui mikataba itatubana ondoka na makaratasi yako hapa yale madini ni ya kwetu, mwanasiasa unayetaka kulia ulie tu na ufe madini hakuna kwenda”, alisema Askofu Gwajima kwenye mahubiri yake jumapili iliyopita kwenye kanisa la ufufuo na uzima, Jijini Dar es salaam.

Kwa upande mwingine Askofu Gwajima amewashambulia watanzania kwa kusema wamerogwa kwani viongozi wake wanasaini ovyo mikataba isiyo na faida huku akidai hata wananchi pia hawafikirii cha kufanya kwani kuna mito mingi lakini wanaacha maji yakitiririka badala ya kuyatumia kwa kilimo.