Monday 31 July 2017

ZITTO Kabwe Awapa Somo Wanaopinga MITAA Kupewa Majina ya Wachezaji

Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amewataka wanao lalamika juu ya baadhi ya mitaa ya Kigoma kupewa majina ya wachezaji wa kikosi cha Taifa Stars kilicho shiriki AFCON mwaka 1980 waache ubinafsi.

Wachezaji wa Stars mwaka 1980 wapatiwa majina ya Mitaa

Zitto ameyasema hayo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Facebook

Nimesikia malalamiko ya baadhi ya watu kuhusu kuipa baadhi ya Mitaa yetu majina ya wachezaji wa Taifa Stars ya mwaka 1980 iliyoshiriki AFCON Lagos.

Lalamiko kubwa ni kwamba kwanini tutoe majina ya watu ambao sio wa Kigoma kwenye Mitaa ya Kigoma Ujiji. Nataka kuwaambia watu hao kuwa kuna watu wa Kigoma wana majina kwenye miji mingine.

Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha ni heshima ya Sheikh Amri Abeid Karuta wa Ujiji. Unapokataa Peter Tino asipewe jina Kigoma unasema na Arusha nao wafute jina la Uwanja. Hoja Hii ni nyepesi na iliyojaa ubinafsi na upofu wa kuona mambo.

Taifa Stars ya Mwaka 1980 itakuwa na mitaa 25 tu. Pia haina maana kuwa watu wengine waliocheza mpira hawatapewa majina. Huwezi kuwa na mitaa Kigoma bila Edibily Jonas Lunyamila ama Nteze John Lungu.

Unawezaje kumwacha Juma Kaseja ambaye amekuwa Nahodha wa Taifa Stars miaka 10? Unamwacha vipi Mavumbi Omar, Kitwana na Kasim Manara? NK. Ieleweke tu kwamba hawa wa Taifa Stars ya mwaka 1980 watakuwa eneo Moja wakati wengine watakuwa sehemu tofauti.

Mfano Kata ya Bangwe wamependekeza jina la Shem Karenga kwenye moja ya mitaa ya Kata hiyo. Watu wengi watapewa mitaa. Viongozi wetu wa Dini waliopita kama Almarhum Sheikh Tofiki Ibrahim Malilo, Sheikh Khalfan Kiumbe, Sheikh Idi Kiburwa, Askofu Kahurananga, Askofu Gerald Mpango nk. Wabunge wote wa zamani wa Wilaya ya Kigoma na Kigoma Mjini.

Wakuu wa Mikoa wa Zamani waliohudumu Kigoma na Mameya wa zamani. Wazee wetu Viongozi wa Kisiasa Kama Mzee Lukandamila, Mzee Nayingo, Mzee Kasisiko, Mzee Menge. Pia Viongozi wa Kitaifa na Kimataifa Kama vile Prof. A M Babu, Che, Josina Machel, Titi Mohammed, Mwami Ntare, Kassim Majaliwa nk. Wafanyabiashara maarufu wa Kigoma na watu wengine waliochangia Kwa njia mbalimbali maendeleo ya Kigoma.

Kuna watu wana mchango maalumu Kwa kigoma na sio watu wa Kigoma lazima kuwaenzi, mtu Kama Sam Ruhuza unawezaje kuacha kumuenzi japo Kwa Mtaa? Mzee Bella Karumba? Shein ? Jaffer?

Hili ni zoezi kubwa na sio la Taifa Stars tu.

Ni zoezi la kutambua mitaa Kwa majina na vibao vya mitaa. Tunaishukuru kampuni ya MihanGas Kwa kukubali ombi letu la kudhamini vibao vya Mitaa Manispaa nzima. Majina ya Mitaa yanaendana na usafishaji wa mitaa pia ili kuwa na mji msafi na endelevu. Kidogo tutafika, hata Mbuyu ulianza Kama Mchicha, alimalizia Zitto Kabwe.