Wednesday 26 July 2017

Mkuu wa wilaya aanzisha kampeni ya kupima mimba mashuleni

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Ndg Chelestino Mofuga amezindua kampeni ya kupima mimba wanafunzi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha hakuna wanafunzi wajawazito na waliozaa kuendelea na masomo katika mfumo wa kawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Ndg Chelestino Mofuga akiongea na wanafunzi

Mofuga amesema kampeni hiyo itawasaidia kurejesha maadili kwa jamii kwa kuacha kufanya ngono na wanafunzi.

Kampeni hiyo inayoitwa ‘Mbulu bila mimba za wanafunzi inawezekana tuwaache wasome’ inalenga kuwafikia wasichana wote wenye uwezo wa kuzaa na kwamba itakuwa endelevu.

“Serikali haina mpango wa kusomesha wanafunzi wajawazito hivyo nawataka mabinti msikubali kudanganywa,”amesema Mofuga kwenye mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi.

Mkuu huyo wa wilaya amewaagiza pia wakurugenzi na wakuu wa shule kuwapima wanafunzi kila baada ya miezi mitatu na kwamba watakaobainika watakuwa wamejifukuzisha shule wenyewe huku amewaonya walimu na wananchi wenye uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi kuacha mara moja kwani wakibainika watakwenda jela miaka 30 bila huruma.

Mofuga pia amewataka walimu wakuu kusimamia taaluma na nidhamu na kuwafichua wazazi wanaokwamisha maendeleo ya wanafunzi shuleni kwa kuwatuma kuchunga ng’ombe siku za shule au kufanya biashara pamoja na wazazi wanaoficha wahalifu wa mimba au kukubaliana kuwaozesha.