Friday 16 January 2015

DARASA LA MAHABA...!!!! MWAKA HUO UNAANZA KUSOGEA, UNAENDELEA KUISHI KWENYE PENZI LA GIZA?

WIKI iliyopita tuliianza mada hii ambayo inatufundisha juu ya umuhimu wa kujitambua kupitia makosa tuliyoyapitia, leo tunaimalizia.
Hakuna sababu ya kuishi katika penzi ambalo halina muelekeo mzuri wa baadaye kama ulivyoishi mwaka jana, ni bora kujiengua na kusubiri kumpata yule atakayetambua thamani ya penzi lako na kupanga mipango endelevu.
Kwa wale tuliokuwa pamoja, tuliishia kwenye kipengele cha TATIZO SUGU. Nilieleza namna ambavyo ulikuwa na tatizo sugu mwaka jana, mwaka huu uliepuke.
Endelea...
Ifike wakati uamue moja, tatueni tatizo katika njia stahiki na kama inashindikana basi si vibaya kila mmoja akaanza kuangalia ustarabu mwingine.
Kama mligombana kiasi cha kutosalimiana au kutoheshimiana, mwaka huu uwe na mabadiliko katika tatizo lako sugu, malizana nalo mapema. Usikubali mwaka huu uwe wa majaribio kama ilivyokuwa miaka mingine.
Kama inawezekana, malizeni kikwazo ili muweze kutazama hatua nyingine ya penzi lenu na kama haiwezekani basi bora mkasitisha safari yenu.
WEKENI MALENGO
Kama nilivyotangulia kueleza, hakuna kitu kinachofanikiwa bila ya kukiwekea malengo. Ukishakuwa umetafakari juu ya mtu uliyenaye na kuona ni sahihi au si sahihi basi ni wakati wako sasa kuanza kujiwekea malengo mapya kwa mwaka huu.
Kama uliye naye umeshamtafakari na kuona mnaendana, basi ni vizuri mkaanza kuzungumzia malengo ya penzi lenu. Kama mmeshadumu kwenye uhusiano kwa muda mrefu, jadilini kuhusu ‘future’ ya penzi lenu. Wekeni malengo kwamba, ndani ya mwaka huu lazima tuwe tumefanikisha jambo fulani.
Muweke malengo na  myatekeleze kweli.  Msikubali yapotelee hewani, tafuteni njia ya kuyafanikisha. Kama ni kuvalishana pete, mvalishane.
Kama ni suala la ndoa basi lazima mjue lina taratibu gani. Mjue njia za kupita ili muweze kutimiza mahitaji yote ya ndoa katika wakati ambao mmejipangia.
FANYA MAAMUZI MAGUMU
Kama uliyenaye unaona hamfanani, haendani na falsafa ya maisha yako, usiogope kuchukua maamuzi magumu. Ni bora ukaamua kuachana naye ili ubaki huru na kusubiri au kutafuta mtu ambaye ni sahihi kwako. 
Usikurupuke kumtafuta mwingine. Tafakari kwa kina kabla ya kufanya maamuzi. Mshirikishe Mungu katika malengo yako. Muombe akusaidie ili uweze kuyafanikisha. Kama umeamua kwa dhati kutafuta mwenzi wa maisha basi kwa imani yako muombe akuoneshe. Umuone katika macho ya kawaida na hata ya kiroho.
JIFUNZE KUPITIA ULIKOTOKA
Jifunze kupitia aina ya maisha uliyopitia awali. Kama ulikuwa mtu wa kutotulia, jisahihishe na uanze safari mpya. Usijutie kuhusu maisha uliyoyapitia bali angalia kule unapokwenda.
Hakikisha unajipangia mwisho mzuri ili mapito yako yabaki kuwa historia na kuwa somo kwa wengine.
JENGA PICHA YA MBALI
Ili uweze kufikia malengo yako, jenga picha ya mbali na si kutazama karibu. Vuta picha ya ndoa unayotaka kuifunga. Vuta picha ya aina ya familia ambayo unataka kuishi. Jiwekee picha ya familia bora yenye watoto wenye nidhamu, wenye maadili na mtakaoweza kuwasomesha katika shule nzuri.
Ukijiwekea malengo ya mbali na makubwa, hakika utachakarika ili uweze kuyatimiza. Utaweza kujifunza kupitia kwa mifano ya watu mbalimbali waliokutangulia, ukachuja na kupata uelekeo mzuri wa kufanikisha kile ulichokifikiria.