Tuesday 16 September 2014

KUHUSU MADAI.YA.KUPINGA BUNGE LA KATIBA LISIENDELEE MAHAKAMA YAWEKA NGUMU

MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar
es Salaam jana imetupilia mbali maombi
ya pingamizi la awali la kusimamisha
Bunge la Katiba linaloendelea mjini
Dodoma, iliyofunguliwa na Mwandishi
wa Habari Said Kubenea, kwa kuwa
wametumia kifungu cha sheria kisicho
sahihi.

Kadhalika, mahakama hiyo imetupilia
mbali pingamizi hilo la awali, kwa kuwa
mlalamikaji ametumia kifungu cha sheria
namba 2 kidogo cha (2) (JALA) ambacho
hakina mamlaka ya kufungua maombi
hayo mahakamani.
Uamuzi huo ulitolewa chini ya jopo
lililoketi la majaji watatu, wakiongozwa
na Mwenyekiti Mh.Jaji Augustino
Mwarija, Dr. Fauz Twaib na Aloyisius
Mujuluzi.
Jopo hilo lilisema mahakama imetupilia
mbali pingamizi hilo la awali kwa sababu
halina mashiko ya kisheria.
Upande wa mlalamikiwa uliongozwa na
Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata
na mlalamikaji Peter Kibatala.
Awali, Mwanasehria Mkuu (AG) kupitia
Naibu Mwanasheria Mkuu, George Masaju
kuiomba mahakama hiyo kutupilia mbali
pingamizi hilo kwa kuwa maombi yake ni
batili kisheria na hayawezi kuthibitishwa
mahakamani, hivyo yatupiliwe mbali.
Katika pingamizi hilo lililoambatana na
hati ya kiapo, AG kupitia naibu wake,
amedai kuwa maombi hayo ya
mlalamikaji yana dosari ambayo haiwezi
kurekebishika kwa kuwa zinahitaji
kifungu maalum cha sheria kinachoipa
nguvu mahakama ya kuridhia maombi
hayo.
Mapema mahakamani hapo, Kubenea
aliwasilisha maombi ya pingamizi la awali
ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda
yaliyopewa usajili wa namba 29 ya mwaka
2014, pamoja na maombi ya msingi ya
tafsiri ya mamlaka ya Bunge yote
yalifunguliwa mahakamani hapo jana
chini ya Hati ya Dharura.
Katika kesi ya msingi iliyopewa usajili
namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea
anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri
sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba
chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya
Sheria ya Marekebisho ya Katiba namba
Namba 83 ya mwaka 2011.
Pamoja na mambo mengine katika kesi
hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya
Bunge hilo, pia Kubenea amewasilisha
maombi mahakamani hapo akiiomba
mahakama itoe zuio la muda la
kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri
uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.