Friday 16 June 2017

Wagosi wa Kaya wafunguka kuhusu ‘Jipu Tumbua’

Kundi la muziki la Wagosi wa Kaya limesema wimbo wao mpya ‘Jipu Tumbua’ umelenga kutetea rasilimali za nchi na kuunga mkono jitihada za Rais John Pombe Magufuli za kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi.



Msanii wa kundi hilo Dokta John amesema katika wimbo huo, wametumia lugha ya staha ambayo haitamvunjia mtu heshima, pia wamekosoa pamoja na kusifia panapostahili.

“Tumbua Jipu ni mlolongo na mpango mzima ambao kama mnakumbuka Mwl. Nyerere alisema tusichimbe madini hadi tupate wasomi kwanza. Kiukweli nchi za nje hawana material haya, kwa hiyo wao wanachimba halafu wanaenda kufanya mambo yao, wanatengeza hela halafu sisi tunaenda kuwapigia magoti kuomba misaada, kwa hiyo wao wanakuwa wanacheza na akili zetu wakati sisi tuna utajiri mkubwa.

“Hivi si vitu vya kuchukulia poa, kwa hiyo unapoona Mheshimiwa anapigana na hii hali, anahitaji sapoti ili tuweze kuona tunanufaika vipi na kizazi kijacho, tusijiangalie sisi tuangalie kizazi kijacho” Dokta John amekiambia kipindi cha Ladha 3600 cha E FM.

“Unajua Wagosi wa Kaya kuhusiana na mlindimo ambao tunaenda nao, hili ni game letu, game la kuongea ukweli, wanaposifia, twasifia kama kimefanyika kitu kizuri kama tunavyoona Mheshimiwa na mambo yanavyokwenda. Kwenye kukosoa tutakosoa kwa sababu sisi tupo katika jamii na tunatumia lugha nzuri sio kuongea zile lugha za kebehi zinazoweza kumfanya mtu mzima kuona amekosewa adabu,” ameongeza.