Thursday 15 June 2017

Makamu wa Rais Samia Suluhu mgeni rasmi mechi ya Everton vs Gor Mahia

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan amekubali ombi la kuwa mgeni rasmi katika mchezo kirafiki kati ya Timu ya Everton ya nchini Uingereza na timu ya Gor Mahia ya Kenya ambayo ilitwaa kombe la michuano ya Sportpesa iliyofayika hapa nchini wiki iliyopita.

Mkurugenzi wa SportPesa Tanzania, Abbas Tarimba na CEO wa SportPesa wakimkabidhi Jezi Makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amekubali ombi hilo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Watendaji wa Kampuni inayojishughulisha na ubashiri ya SportPesa nchini ambao waliongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji Bwana Tarimba Abbas Ikulu- Dar es Salaam.

Mama Samia Suluhu amepongeza mipango na mikakati mizuri ya kampuni hiyo ya kutaka kukuza vipaji vya wanamichezo hasa kwa mpira wa miguu kwa Tanzania Bara na Zanzibar na kusema kama malengo hayo yatafikiwa Tanzania itakuwa bora katika mchezo wa mpira wa katika bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.

Makamu wa Rais pia amewahakikishia watendaji wa kampuni hiyo kuwa milango ya ofisi yake ipo wazi na pindi wakiwama katika jambo lolote wawasiliane na ofisi yake ili tatizo linalowakabili liweze kutafutiwa ufumbuzi ili lisikwamishe shughuli za kampuni hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya SportPesa nchini Tanzania, Tarimba Abbas amemweleza Makamu wa Rais kuwa kampuni hiyo ina malengo makubwa ya kufanya biashara hapa nchini kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchini.



Tarimba amesema katika mipango yao wanataka katika kipindi cha miaka Mitatu ijayo kampuni yao iwe ni moja ya kampuni bora nchini katika ulipaji wa kodi kwa Serikali kama wanavyofanya kwa sasa katika Serikali ya Kenya.

Amesema mipango na mikakati waliyonayo kwa sasa ni kuhakikisha wanainua vipaji vya wanamichezo nchini kwa sababu Tanzania Bara na Zanzibar kuna vipaji vingi vya wachezaji wa mpira wa miguu ambavyo haviendelezwi ipasavyo.

Watendaji wa Kampuni hiyo pia wamemshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kukubali ombi lao na kuwa Mgeni rasmi katika mchezo wa kirafiki kati ya Timu ya Everton ya nchini Uingereza na timu ya Gor Mahia ya Kenya mchezo ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 13 Julai mwaka huu katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya SportPesa nchini, Tarimba Abbas amesema moja ya lengo la kuileta Timu ya Everton nchini ni pamoja na mambo mengine ni kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii nchini kupitia mchezo huo ambao unatarajiwa kuangaliwa na maelfu ya watazamaji Duniani kote.

Mkurugenzi huyo pia amemweleza Makamu wa Rais kuwa tayari wameshawasiliana na mamlaka inayohusika na masuala ya utalii nchini ili iweze kutumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini kama hatua ya kuongeza idadi ya watalii watakaokuja kutembelea vivutio nchini na kuongeza mapato ya Serikali kupitia sekta hiyo.

Mechi ya Everton na Gor Mahia inatarajiwa kuchezwa mwezi July tarehe 13 mwaka huu kunako dimba la Taifa jijini Dar es salaam, Tanzania.