Friday 16 September 2016

VISA VYA HUYU KIUMBE MWANAUME!

'
Kwenye swala la mapenzi wanaume hawana mzaha'
Katika Gazeti la Mwananchi la hivi karibuni la May 18, 2010, kuna habari iliyoandikwa na mwandishi Anthony Kayanda wa Kigoma ambayo ilinisikitisha sana. Habari yenyewe ni ile iliyohusu mtu mmoja kuuwawa kwa kuchomwa kisu kifuani kwa tuhuma za kutembea na mke wa mtu.Kwa mujibu wa Gazeti hilo, tukio hilo limetokea katika kijiji cha Kitagata kilichopo katika tarafa ya Makere, Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.



Marehemu ametajwa kuwa ni Ally Bwisigwa ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.Ilidaiwa kwamba Marehemu alikuwa akitembea na mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Perusi ambaye aliwahi kuolewa na Hassan Rashid mkazi wa Kasulu Mjini na waliishi pamoja kwa muda mrefu kabla ya mume huyo kufungwa gerezani.Baada ya mumewe kufungwa, Perusi alirudi kijijini kwao huko Kitagata na ndipo alipoanza mahusiano ya kimapenzi na marehemu.





Inadaiwa kuwa baada ya Mume huyo kutoka Gerezani alimuonya mtuhumiwa mara kadhaa kuacha kutembea na mkewe lakini marehemu aliendelea na mchezo wake huo mchafu.Inadaiwa kuwa Hassan alifanya majaribio mawili ya kutaka kumuua marehemu kwanza kwa kutaka kumgonga na pikipiki na tukio la pili lilikuwa ni lile la kumchoma kisu ambapo hata hivyo kisu hicho hakikumpata.







Nimesema kuwa tukio hilo limenisikitisha sana kwa sababu bado nashindwa kuelewa hivi inakuwaje mpaka mtu unapoteza maisha kwa sababu ya mwanamke, tena kibaya zaidi mke wa mtu!Ingawa inasemwa kwamba wanawake ni viumbe wa ajabu lakini naamini wanaume ndio viumbe wa ajabu kupindukia.







Kwa nini ninasema hivyo? Ninasema hivyo kwa sababu, wanawake kwa ujumla wao wanavyo vibweka vyao katika swala zima la mapenzi, lakini ukija kwa wanaume naamini nao wanavyo vibwekwa vyao tena vya hatari ukilinganisha na vile vya wanawake.Kwa mfano, hivi ni mara ngapi tumeshawahi kusikia baadhi ya wanaume wakiamua kujinyonga kwa sababu ya kushindwa kuwashawishi wanawake wanaowapenda?







Namini kuwa matukio ya aina hiyo yapo sana na sio kwa huko nyumbani tu bali pia hata katika nchi zilizoendelea. Linapokuja swala la mapenzi kuna baadhi ya wanaume wanakuwa kama Nyati waliojeruhiwa, na ndio sababu unaweza kukuta baadhi ya wanaume wanajiingiza kwenye vitendo viovu kama vile vya wizi au ujambazi kwa lengo la kuwashawishi wanawake wanaowapenda ili wawakubali. Wakati mwingine hujiingiza kwenye matumizi ya Pombe kupita kiasi au hata matumizi ya Bangi na madawa ya kulevya kutokana na kuachwa na wanawake wanaowapenda.







Tabia hii ya wanaume kuhatarisha maisha au hata kupoteza maisha kama tulivyoona katika tukio hilo la Kigoma ni la tangu enzi za kale. Kuna simulizi nyingi tulikuwa tukisimuliwa enzi za utoto wangu huko nyumbani kwamba kuna wakati wanaume walikuwa wakipigana ili kumgombea mwanamke na shujaa anayeshinda katika ugomvi ndiye anayemchukuwa mwanamke anayegombewa.







Inaonekana wazi kwamba uwezekano wa mwanaume kufa mapema au kuhatarisha maisha yake ni mkubwa ukilinganisha na ule wa wanawake. Na hiyo inatokana na wanaume kupenda sifa na kutaka kuwamiliki wanawake wawapendeo. Kuna matukio mengi ya kusikitisha ambayo huwa tunayasoma katika vyombo vyetu vya habari ambapo matukio kama yale ya mwanaume kumuua mwanaume mwenzie ili kumpata mwanamke ampendae ni vya kawaida kabisa.







Kwa mfano katika tukio hilo la Kigoma, licha na kukoswa koswa kuuwawa mara mbili lakini marehemu hakukoma kutembea na mke wa mwenzie, mpaka akasababisha kupoteza maisha.Hivi kumekuwa na uhaba wa wanawake kiasi cha kupelekea baadhi ya wanaume kuhatarisha maisha yao au kupoteza maisha kutokana na kumgombea huyu kiumbe mwanamke au kuna kitu kingine kinachotafutwa hapo?



Ni aghalabu sana kusikia mwanamke kamuua mume baada ya kumfumania au kumuua mgoni wake tofauti na wanaume. Kama ukipima jambo hilo kitakwimu basi utapata idadi ya wanaume ya kutosha ukilinganisha na ile ya wanawake.







Kimsingi wanaume wamewageuza wanawake kama mali zao wanazozimiliki na hiyo ndio sababu inapotokea kumfumania mkewe au mchumba wake akiwa na mwanaume mwingine mambo mawili yanaweza kutokea, kwanza atamuadhibu mgoni wake au hata kumuua kisha mke naye atasulubiwa au hata kuuawa.




Lakini, pale anapofumaniwa mwanaume mambo huwa ni tofauti sana. Kuna uwezekano mkubwa wa mke huyo kusulubiwa kwa sababu amemfumania mume na wakati mwingine hata huyo mgoni anaweza kushirikiana na mume huyu kumuadhibu huyo mwanamke aliyefumania.Nadhani kuna haja ya wanaume kujikagua upya na kubadili mwenendo wao mzima juu ya matendo yao ili kuepuka kupoteza maisha kwa jambo ambalo wangeweza kuliepuka.