Sunday 8 February 2015

MWANAMKE MZURI ANAPASWA KUWA NA VIGEZO GANI?

Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa, ni Jumatatu nyingine ninapokukaribisha kwa moyo mkunjufu kwenye busati letu la mahaba, tukijuzana na kuelimishana mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa
kimapenzi.
Leo nataka tujadiliane kuhusu mada ambayo siyo ngeni lakini imekuwa ikisababisha mivutano na migongano mingi ya kimawazo mara kwa mara kila inapojadiliwa, hasa na wanaume au wanawake wenyewe.
Hivi umeshawahi kujiuliza mwanamke mzuri anapaswa kuwa na vigezo vipi? Tukizungumzia mwanamke mzuri, kichwani mwako unajenga taswira gani?
WENGI WANADANGANYIKA NA SIFA ZA NJE
Ukipata nafasi ya kuzungumza na wanaume na kuwauliza wanawake wazuri wakoje, majibu utakayoyapata yatakushangaza. Wengi watazungumzia wanawake wenye sura nzuri, weupe sana, weusi wenye mvuto, wenye maumbo yanayokaribia kufanana na namba nane au ‘waliojazia’.
Ndiyo, wengi wanashindwa kuutathmini uzuri wa mwanamke kwa sifa za ndani isipokuwa zile za nje ambazo ni rahisi kuziona. Matokeo yake, wanawake wanaokosa sifa hizi kama nilivyozitaja hapo juu, wanajihisi hawana thamani katika jamii. Wengine wanafikia hatua ya kununua dawa za Kichina ili kutengeneza shepu na wao waonekane wazuri na wanaovutia mbele ya macho ya wanaume.
Wengine wanaenda mbali zaidi kwa kudiriki hata kununua nguo za ndani zilizoshonewa ‘masponji’ ili tu waonekane wamejazia. Wengine wanajiharibu ngozi zao za asili kwa kujipaka vipodozi vikali ilimradi nao waonekane weupe na wenye kuvutia.  Wanasahau kwamba uzuri wa mwanamke, siyo sura wala umbo bali ni zile sifa za ndani alizonazo mtu.
NI KWELI WANAWAKE WAZURI HAWAOLEWI?
Hili ni swali lingine linaloweza kukupa majibu kwamba mwanamke mzuri ni yupi. Ni hulka ya wanaume wengi kuwa na wanawake ‘wazuri’ katika maisha yao. Hata hivyo, hapohapo, upo ushahidi wa wanawake wengi ambao jamii iliamini kwamba ni wazuri lakini mpaka leo wanasota mitaani bila ndoa.
Kama kila mwanaume anatamani kuishi na mwanamke mzuri, kwa nini kundi hili halipati wanaume wa kuwaoa kwa urahisi? Ni hapo ndipo unapotakiwa kujiongeza kuwa kumbe uzuri wa mwanamke siyo sura, rangi ya ngozi yake wala shepu yake
bali kuna kitu kikubwa zaidi ya hicho.
VIGEZO VYA UZURI VIKO TOFAUTI KABISA
Hujawahi kukutana na mwanaume ambaye amemuoa mwanamke ambaye watu wake wa karibu kila wakikaa wanaulizana ‘hivi alimpendea nini huyu? Mbona hawafanani?’
 Ipo mifano ya wanaume wengi ambao baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kusaka wenzi wa kuishi nao na kuanzisha familia, mwisho waliishia kwa wanawake ambao hawana ‘uzuri’ ambao jamii nzima inautafsiri kuwa ndiyo uzuri anaopaswa kuwa nao mwanamke.
Mwonekano na sifa za nje, hivyo vyote ni vya ziada tu na ndiyo maana wapo wanawake ambao hawana sifa hizo lakini wameolewa na wanaume wa maana na kudumu kwenye ndoa zao huku wale wenye sifa na vigezo vya nje, wakiishia kubadilisha wanaume kila kukicha mitaani, wengine wakifikia hata hatua ya kujiuza. Kwa maelezo hayo, utakubaliana na mimi kwamba kumbe vigezo vya mwanamke mzuri, viko tofauti kabisa na unavyofikiri.
Sasa kumbe mwanamke mzuri anapaswa kuwa na vigezo gani? Ni sifa zipi zinazofanya mwanamke aolewe na kudumu kwenye ndoa yake hata kama hana sura au shepu nzuri?
Naamini wewe msomaji wangu unajua zaidi, naomba tuchangie mawazo. Tuma ujumbe wako kwa namba za hapo juu na unieleze kwa mtazamo wako mwanamke mzuri ni yupi na anapaswa kuwa na vigezo gani.