Sunday 12 August 2018

'MSITUTISHE" Uturuki yasema haiogopi vitisho vya Marekani

Rais Recep Tayyip Erdogan ameapa kutotii vitisho vya Marekani kuhusiana na mchungaji anaezuwiliwa nchini Uturuki, huku mzozo baina ya washirika hao wa NATO ukizidi, na kusababisha kuporomoka sarafu ya Uturuki la Lira.

Rais huyo wa Uturuki alisema pia kuwa ushirika wa nchi yake na Marekani unaweza kuwa katika hatari, akionya kuwa Ankara huenda ikaanza kutafuta washirika wapya, katika makala ya maoni alioiandika katika gazeti la New York Times.

Uhusiano kati ya washirika hao wakubwa wa NATO umeshuka kwa kiwango cha chini kabisaa katika ipindi cha miongo kadhaa, kuhusiana na mkururu wa masuala, yakiwemo kuzuwiliwa kwa mchungaji wa Kimarekani Andrew Brunson kwa tuhuma za ugaidi, na kupelekea thamani ya sarafu ya Uturuki ya Lira kuporomoka dhidi ya dola.

Sarafu ya Lira ilishuka kwa asilimia 16 dhidi ya dola siku ya Ijumaa, na kushuka zaidi baada ya rais wa Marekani Donald Trump kusema ameongeza maradufu viwango vya kodi vinavyotozwa kwenye bidhaa za chuma na bati kutoka Uturuki.

"Ni makosa kuthubutu kuifanya Uturuki isalimu kuptia vitisho kuhusiana na mchungaji," alisema Erdogan katika mji wa bahari nyeusi wa Unye. "Hamna haya, hamna haya," alisema katika matamshi yake yalioelekezwa moja kwa moja kwa serikali mjini Washington. Mnabadilishana mshirika wenu wa kimkakati kwa mchungaji."

Trump alitangaza viwango hivyo vya adhabu kupitia mtandao wa Twitter, akisema "Uhusiano wetu na Uturuki siyo mzuri kwa wakati huu!" Ikulu ya White House imesema vikwazo vipya vilivyowekwa vitaanza kutekelezwa Agosti 13.